Mvua Yasababisha Vifo Vya Watoto Wawili

KITAIFA

WATOTO wawili wa familia moja wamefariki dunia huku watu 77 wakazi wa kijiji cha Mibungonanakwekwe wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wakikosa makazi baada ya nyumba zao 16 kubomolewa kwa mvua iliyoambatana na upepo mkali.

Watoto waliokufa katika tukio hilo baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba walimokuwa wamelala wametambuliwa kuwa ni Nelson Benedictor (3) na Daison Benedictor mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu .

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Mulilo Jumanne Mulio amesema tukio hilo lilitokea jana saa 9:00 usiku wa kuamkia Februari 25.

Alisema watu wengine wa familia hiyo, Mektrida Benedictor (30) na Eric Benedictor (7) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya msingi Namakwekwe wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo mjini Nansio kwa matibabu.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Ukerewe, Dk Revocatus Cleophace alisema majeruhi katika tukio hilo wanaendelea vema na miili ya watoto waliopoteza maisha imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini hapo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *