Masauni : Tutasimamia Maadili Ya Polisi

KITAIFA

Serikali imesema kuwa haitakuwa tayari kuona Jeshi la Polisi linachafuliwa na baadhi ya askari Polisi wasiofuata maadili huku ikisisitiza haitosita kumchukulia hatua askari atakayebainika kukiuka maadili

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni wakati akifunga mafunzo kwa Vikundi vya Ulinzi Shirikishi Visiwani Zanzibar ambapo jumla wa walinzi 681 walihitimu mafunzo hayo

Amesema kuwa Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na askari polisi waadilifu huku akiweka wazi kuwepo kwa askari wasio waadilifu

“Jeshi letu la Polisi lina miiko yake katika utendaji wa kazi zake,lakini wapo askari wachache wanaovujisha taarifa kwa wahalifu, wanasaidia wahalifu kutenda makosa sambamba na kupokea rushwa,hali hiyo haikubaliki na atakayebainika hatutosita kumchukukia hatua kwa mujibu wa taratibu za jeshi,” amesema Masauni

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Saleh Mohamed Saleh, amewataka wananchi kufichua wahalifu wanaowafahamu katika makazi yao ili matendo ya uhalifu yaweze kupungua

Katika mafunzo hayo jumla ya Walinzi Shirikishi 681 walihitimu ambapo walipitishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ukamataji salama, namna ya kuendesha doria jinsi ya kumfikisha mtuhumiwa kituo cha polisi na elimu jinsi ya kujikinga na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *